Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma watakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuongeza ubunifu katika kutekeleza majukumu yao

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Nyakimura Muhoji ametoa wito kwa watumishi wa Tume kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na misingi ya Utawala bora.

Bw. Nyakimura Muhoji amesema hayo katika hafla ya kumuaga Bibi Mary Kilo ambaye amestaafu Utumishi wa Umma kwa mujibu Sheria, hafla iliyofanyika Agosti 27, 2014. “Ili Utumishi wa Umma uweze kukidhi matarajio ya wananchi ya kupata huduma bora na kwa wakati pamoja na kukuza uchumi wa nchi yetu, Tume inawajibu wa kusimamia vizuri Sheria, Kanuni,Taratibu na Miongozo mbalimbali ambayo husaidia katika kutoa maamuzi na kutenda haki kwa usawa katika Utumishi wa Umma”, amesema.

Aidha, Bw. Muhoji amewaasa watumishi wa Tume kuongeza bidii, moyo wa kujituma na ubunifu katika utendaji kazi. Amesema kwa kufanya hivyo kutawafanya wadau wa Tume kuendelea kuwa na Imani na Serikali yao kwa kuonyesha kuwa inawajali na inatoa haki na usawa kwa kila mtumishi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu wa Tume - Idara ya utumishi wa Afya, Bibi Roseline Mboya alitoa wasifu wa Bibi Mary Kilo kuwa amefanya kazi katika Tume ya Utumishi wa Umma kwa miaka 13 na katika kipindi chote cha Utumishi wake alishirikiana vizuri na watumishi wenzake katika utendaji kazi kwa kufanya kazi kwa bidii, kujitoa kwa moyo na hivyo kuwa mfano wa kuigwa kwa watumishi wengine.

Kwa upande wake Bibi Kilo amewaasa watumishi wa Tume kuendeleza moyo wa upendo walionao na kufanya kazi kwa bidii ili Tume iweze kufikia malengo yake iliyojiwekea ikiwemo kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wadau wake.

Aidha, Bibi Kilo ameushukuru uongozi wa Tume ys Utumishi wa umma na watumishi wote kwa kushirikiana naye vizuri katika kipindi chote cha Utumishi wake. Pia amewashukuru watumishi wa Tume kwa zawadi ambazo wamempa. Amesema kuwa zawadi hizo zitakuwa msaada mkubwa kwake katika maisha aliyoyaanza baada ya kustaafu kwa kuwa zitamsaidia katika kujitafutia kipato cha kuweza kumudu kuendesha maisha yake. Miongoni mwa zawadi alizopewa ni seti moja ya kompyuta na printa.

Hafla hiyo imefanyika katika ofisi za Tume ya Utumishi wa Umma, Ubungo Plaza na kuhudhuriwa na baadhi ya watumishi wa Tume. Bibi Mary Kilo amestaafu kwa mujibu wa Sheria mwezi Mei, 2017.

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.