Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Tume ya Utumishi wa Umma yatembelewa na Maafisa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano na Taasisi ya Kupambana na Rushwa Malawi

Tume ya Utumishi wa Umma, tarehe 28 Julai, 2017 ilitembelewa na Maofisa kutoka Taasisi ya Kupambana na Rushwa ya Malawi na Kamati ya Maadili ya Mamlaka ya Mawasiliano ya Malawi, ambao walikuja nchini Tanzania kwa ziara ya siku tano, kuanzia tarehe 24 hadi 28 Julai, 2017, kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu utendaji kazi wa Kamati ya Maadili katika suala la rushwa.

Akizungumza baada ya kuwapokea, Katibu wa Tume, Bw. Nyakimura Muhoji, aliwakaribisha kwa kusema kuwa wao ni majirani zetu, anaelewa wamekuja Tume kwa ajili ya kujifunza jinsi Kamati za Maadili zinavyoendeshwa katika Taasisi yetu, hivyo ujio wao huo uwe ndio mwanzo wa kuweza kukuza mashirikiano baina ya Taasisi hizi.

Wakati wa ziara yao Tume wageni hao walipata fursa ya kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi na Kamati ya Maadili ya Tume kuhusu namna ya kushughulikia masuala ya rushwa. Katika Kikao hicho, Kamati ya Maadili ya Tume ilipata fursa ya kueleza kwa ufupi majukumu ya Tume, Muundo wa Tume na Uzoefu wa Kamati hiyo ya Maadili katika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Mwongozo wa Ufuatiliaji wa Uzingatiaji wa Maadili katika Utumishi wa Umma.

Wakizungumza wakati wa majadiliano ya pamoja Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Mamlaka ya Mawasiliano ya Malawi walieleza kuwa Kamati yao yenye Wajumbe tisa ilianzishwa mwaka 2011 na tangu kuanzishwa kwake haijawahi kufanya uchunguzi wa suala la rushwa. Hivyo, walipenda kufahamu na kupata uzoefu iwapo Kamati ya Maadili ya Tume imewahi kushughulikia suala la mtumishi wa Tume aliyekabiliwa na tuhuma au kosa la kupokea au kutoa rushwa. Kamati ya Maadili ya Tume ilieleza kuwa hakuna mtumishi wa Tume aliyewahi kukabiliwa na tuhuma au kosa la kupokea au kutoa rushwa. Kwa mantiki hiyo, Kamati haijawahi kushughulikia suala la namna hiyo.

Kuhusu ukomo wa utendaji kazi wa Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Mamlaka ya Mawasiliano ya Malawi walibainisha kuwa muda uliowekwa kisheria ni kipindi cha miaka mitatu. Hata hivyo, walifafanua kuwa Sheria yao haijaweka wazi endapo mjumbe wa kamati hiyo anaweza kuteuliwa tena baada ya kumalizika kwa muda huo. Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Mamlaka ya Mawasiliano Malawi walitaka kufahamu Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma Tanzania zinatumika katika makundi gani ya Utumishi.

Naibu Katibu, Idara ya Utumishi Serikalini katika Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Richard Odongo alifafanua “Kwa mujibu wa maagizo ya Katibu Mkuu Kiongozi, Kanuni hizo za Maadili zinatumiwa na watumishi walioko katika Utumishi wa Serikali Kuu, Utumishi wa Walimu, Utumishi wa Serikali za Mitaa, Utumishi wa Afya, Wakala za Serikali, Taasisi za Umma na Watumishi wa Serikali wenye masharti ya kawaida. Kanuni hizo hazitumiki kwenye majeshi. Pamoja na Kanuni hizo zipo pia Kanuni za maadili ya kitaaluma mfano kwa Wataalam wa Afya na Walimu” alisema.

Kuhusu utaratibu unaotumiwa wa kumlinda mtoa taarifa ya masuala ya rushwa, alisema kuwa mfumo wa utendaji kazi wa Tume hauruhusu mtumishi yeyote wa Tume kutoa taarifa za siri. Pia upo mfumo wa kuwasilisha taarifa kwa njia ya sanduku la maoni ambapo mtoa taarifa anaweza kuwasilisha taarifa yake bila kuweka wazi jina lake.

Aidha, Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Mamlaka ya Mawasiliano Malawi walipenda kufahamu kama Kamati ya Maadili ya Tume inayo bajeti ya kutekeleza majukumu yake, ambapo walielezwa kuwa inatekeleza majukumu yake kwa kutumia bajeti ya Tume baada ya Kamati hiyo kuwasilisha mahitaji yake kwa Katibu wa Tume.

Wajumbe hao kutoka Malawi, waliishukuru Tume kwa mapokezi mazuri na walieleza kuwa wamejifunza mengi kupitia ziara yao waliyoifanya katika Tume na waliwakaribisha Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Tume kutembelea Ofisi zao zilizopo Blantyre, Malawi ili kubadilishana uzoefu zaidi wa masuala mbalimbali ya kiutendaji katika Utumishi wa Umma.

Kwa upande wake Bibi Tunu Mleli, mwakilishi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) aliishukuru Tume kwa kufanikisha ziara hiyo licha ya Tume kuwa na ratiba ya kazi nyingine muhimu.

Hapa nchini, wenyeji wa ugeni huu walikuwa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na Taasisi zilizotembelewa ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Tume ya Ushindani na Tume ya Utumishi wa Umma.

Maofisa walioshiriki katika majadiliano hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Tume, Ubungo Plaza kutoka Mamlaka ya Mawasiliano ya Malawi ni Bibi Ivy Fossa, Bw. Kalimwayi Kaliya, Bw. Joseph Ngalawa, Bw. Hery Macheso, Bibi Diana Ziwoya na Bibi Ivy Chpezaari. Kutoka Taasisi ya Kupambana na Rushwa ya Malawi ni Bibi Susan Phiri. Kwa upande wa Tume ya Utumishi wa Umma walikuwa ni Naibu Makatibu,  Bibi Rose Elipenda (Idara ya Utumishi wa Serikali za Mitaa)  na Bw. Richard Odongo (Idara ya Utumishi Serikalini); Makatibu Wasaidizi  Bw. John Mbisso, Bibi Evalyne Omari na Bibi Selina Maongezi, pamoja na Afisa Habari wa Tume, Bi Jorlin Kagaruki. Aidha, wageni hao waliongozana na Bi Tunu Mleli, Afisa Habari wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

 

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.