Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

WATUMISHI WA TUME YA UTUMISHI WA UMMA WAASWA KUONGEZA BIDII KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Nyakimura Muhoji amewataka watumishi wa Tume kuongeza bidii na maarifa wanapotekeleza majukumu yao, huku akisisitiza Ushirikiano mzuri, Amani na Upendo  ziwe ndio nguzo kuu za kufanikisha majukumu ya Tume yaliyopo kwa ufanisi.

Muhoji aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mkutano wa Tume Ubungo Plaza, wakati alipokutana na kuzungumza na watumishi wa Tume na kuhitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza tarehe 16 hadi 23 Juni, 2017.

Katika maelezo yake, Muhoji alisema ili kufikia malengo ya kufanyika kwa maadhimisho haya, Tume imeweza kutenga siku tatu mahsusi za kukutana na wadau, siku moja kwa Katibu na  Wakuu wa Idara kukutana na watumishi  ili kusikiliza na kufanyia kazi matatizo sugu yanayowakabili wadau pamoja na watumishi na pia kupokea maoni, malalamiko na ushauri  kuhusu uendeshaji na usimamizi wa Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma. Vile vile, imeweza kujitangaza ili kutoa fursa kwa wadau kuelewa zaidi kazi na majukumu ya Tume.

“Tangu nimeteuliwa kuwa Katibu, leo tarehe 23 Juni, nimetimiza miezi minne, wiki mbili na siku mbili, nimeridhika na ushirikiano wenu, tumeshirikiana kwa ukaribu na kiwango cha utendaji kazi kimepanda. Tuongeze bidii zaidi, tuendelee kushirikiana vizuri, Amani na Upendo ziwe ndio nguzo kuu zitakazotuwezesha kufanikiwa katika majukumu yetu kwa ufanisi”

“Nafahamu kuna changamoto mnazokabiliana nazo wakati mkitekeleza majukumu yenu, tuendelee kushirikiana kwa pamoja kuzitatua. Tunafanya kazi kwa kuzingatia bajeti na mtiririko wa rasilimali fedha inayopatikana, ninaahidi nitazifanyia kazi changamoto hizo” alisema Muhoji.

Awali, akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Tume, Bambumbile Mwakyanjala alisema mwelekeo na matarajio ya Tume katika mwaka ujao wa fedha 2017/ 2018, ni kupanua wigo wa Taasisi zinazokaguliwa; Kushughulikia Rufaa na kufanyika kwa Vikao vya Tume kwa wakati pamoja na Kuwezesha wadau. Akizungumzia mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika katika Muundo wa Tume alisema, “ili kuongeza ufanisi Muundo wa Tume unafanyiwa marekebisho kutoka Idara tatu zilizopo sasa na kuwa mbili kuendana na majukumu ya msingi ya Tume, mabadiliko hayo yatapelekea Tume kuwa na Idara ya Ukaguzi na Idara ya Rufaa”.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu, Lington Ngaikwela alitoa wito kwa watumishi wa Tume kuendelea kuiunga mkono Serikali katika vita kubwa iliyopo ya mapambano dhidi ya Rushwa, alisema “Tume kupitia jukumu lake la kushughulikia Rufaa imekuwa ikitenda haki, haijawahi kupindisha uamuzi wake, haijawahi kulalamikiwa na wadau wake kuhusu uwepo wa Rushwa, kutokulalamikiwa ina maana hatuna Rushwa, kwa vile kwetu hatuna Rushwa basi tuendelee kuikemea Rushwa”.

Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) Tawi la Tume, Beatrice Swai, aliushukuru Uongozi wa Tume kwa kuwashirikisha wafanyakazi katika masuala mbalimbali ya utendaji kazi, hali hii imesababisha changamoto mbalimbali zinazojitokeza kutatuliwa sehemu ya kazi.

“Napenda kukupongeza Katibu wa Tume kwa kutenga muda na kutoa fursa kwa watumishi kuweza kukutana na wewe na kutoa maoni, madukuduku (kero) yao, njia hii inaongeza mashirikiano, wafanyakazi  wanaposikilizwa na wanapohusishwa katika masuala muhimu ya utendaji kazi wanakuwa na uelewa mkubwa wa masuala mbalimbali na wao kujiona ni sehemu ya utekelezaji wa malengo yaliyopangwa” alisema.

Kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, kupitia Katibu, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mstaafu) Dkt. Steven J. Bwana, alitoa Salamu za Pongezi kwa Watumishi wa Tume  kwa yale yote yanayotekelezwa na Tume.

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.